Jumuiya ya Taasisi za Vyuo vya
Elimu ya Juu Tanzania(TAHLISO) imewaonya wanaotumia kifo cha Mwanafunzi
Akwilina Akwilini kisiasa huku wakitumia mwamvuli wa jumuiya hiyo kutoa matamko
mbalimbali waache tabia hiyo vinginevyo watachukuliwa hatua.
Aidha,
Jumuiya hiyo imewaomba wanafunzi kuendelea kuwa watulivu kusubiri matokeo
ya uchunguzi wa kifo cha Akwilina na kujiepusha na maandamano na vitendo
vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Onyo
hilo limetolewa leo mjini Dodoma na mwenyekiti wa jumuiya hiyo, George Mnali alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kikao na kamati tendaji ya Tahliso
kwa ajili ya kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Kikao
hicho kimehusisha Marais wa serikali za wanafunzi wa Vyuo hivyo nchini.
Mnali
amesema Tahliso ndio chombo kikuu cha kuwasemea wanafunzi wote nchi nzima na
sio kikundi kingine chochote.
“Vipo
vikundi vingi vimejitokeza na kutoa matamko mbalimbali baada ya kifo hiki cha
Mwanafunzi mwenzetu Akwilina Akwilini kutokea, vikundi vingine vikaenda mbali
zaidi kwa kuwataka baadhi ya watendaji wa serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya
Ndani Kujiuzulu jambo ambalo linaashiria vikundi hivyo kutumika
kisiasa,”amesema
Ameeleza
kuwa haiwezekani kutaka watendaji wa serikali wajiuzulu wakati uchunguzi bado
unafanyika na matokeo ya uchunguzi bado hayajatoka.
“Jambo
la kusikitisha zaidi kuna baadhi ya vikundi vimejitangaza kwamba vinaungwa
mkono na Marais wa Vyuo Vikuu jambo ambalo sio la kweli,”amesema Mwenyekiti
huyo
Ametoa
wito kwa vikundi vyote vinavyojihusisha na kutumia mwamvuli wa Marais wa Vyuo
Vikuu kama kinga yao ilikuuhadaa umma kwamba wanaungwa mkono, viache tabia hiyo
vinginevyo watachukuliwa hatua.
Hata
hivyo amesema Tahliso wanasubiri matokeo ya uchunguzi unaofanyika juu ya kifo
cha Akwilina na wanatumai wahusika wote watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amewaomba
wanafunzi waendelee kuwa watulivu wakati wanasubiri matokeo hayo nakujiepusha
na maandamano na vitendo vyovyote vinavyosababisha uvunjifu wa amani na kuleta
mgawanyo miongoni mwa wanafunzi.
Kadhalika,
amesema namna bora ya kufikisha hoja ni kutumia njia ya majadiliano kama wasomi
badala ya kutumia nguvu ya maandamano kwa kutofuata taratibu na madhara yake ni
kusababisha vurugu zisizotakiwa na hatimaye kuhatarisha usalama na hivyo
kuathiri jamii kwa ujumla wake.
Mnali
amemshukuru Rais John Magufuli kwa kuingilia kati suala hilo la kifo cha
Akwilina na kuagiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa
wote watakaobainika kuhusika na kifo hicho.
0 comments:
Post a Comment