Serikali
imesema ipo tayari kutoa ushirikiano kwa TAWASANET, wanachama wake na wadau
wengine wanaofanya kazi katika sekta ya maji na usafi wa mazingira ili kujenga
misingi ya uadilifu, uweledi na uwajibikaji miongoni mwa Asasi zisizo za Kiserikali.
Hayo yamesemwa leo hapa mjini Dodoma na Naibu
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI )Tickson
Nzunda, wakati akifungua mkutano wa siku mbili wa wadau katika Sekta ya maji na
Usafi wa Mazingira.
Amesema Serikali inatambua na kuthamini jitihada zinazofanywa
na Asasi za Kiraia na wadau wa maendeleo katika kujenga na kuimarisha masuala
ya uwajibikaji kwenye ngazi ya Jamii huku akiwaasa kutumia rasilimali chache walizonazo
kwa maslahi na malengo ya taasisi na siyo maslahi ya mtu binafsi.
Ameongeza kwamba ni muhimu wadau wote kusaidiana na
Serikali katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa kuzingatia vipaumbele vya
Serikali ambavyo ni ujenzi wa Miundombinu ya maji, utunzaji na uhifadhi wa
vyanzo vya maji na usafi wa mazingira.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAWASANET , Herbet Kashilila amesema mkutano huo unalenga kubadilishana uzoefu baina
ya taasisi mbalimbali hasa kwenye dhana ya uwajibikaji wa jamii katika
kuonyesha majukumu na wajibu wa kila ngazi katika utawala wa Serikali.
Mmoja wa wadau
wanaoshiriki katika mkutano huo kutoka shirika la Plan International kupitia
mradi wa usafi wa mazingira Tanzania ( UMATA ) Lydia Mcharo amesema mkutano huo
utawasaidi kutafuta njia nzuri ya
ushirikiano katika kutimiza na kutekeleza malengo ya Sekta ya Maji na Usafi wa
mazingira.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na TAWASANET
ukiwajumuisha wadau kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ambayo hujiusisha na
sekta ya maji pamoja na usafi wa mazingira hapa nchini.
0 comments:
Post a Comment