Umoja wa Afrika (AU) wataka Trump aombe radhi




Umoja wa Afrika (AU) umelaani matamshi ya dharau na kuishushia hadhi Afrika aliyotoa Rais Donald Trump alipokutana na wabunge kwenye ofisi yake ya mviringo ikulu.

Vyombo vya habari vya Marekani yakiwemo mashirika makubwa kama CNN na Washington Post yalinukuu vyanzo vya uhakika kwamba Trump aliyaita mataifa ya Haiti, El Salvador na Afrika kuwa “mataifa machafu”.

Katika kikao hicho Alhamisi iliyopita Trump inadaiwa alihoji: “Kwa nini tunawaruhusu watu hawa kutoka “nchi chafu” kuingia nchini?”

Botswana imekuwa nchi ya kwanza Afrika kumshutumu Trump kwa kuyaita mataifa ya Afrika kuwa "machafu" na ikasema tamko la rais huyo ni la kukosa kuwajibika, linakera na uthibitisho wa "ubaguzi wa rangi".

Pia imechukua hatua ya kumwita balozi wa Marekani aliyeko Botswana aweze kufafanua iwapo Marekani inachukulia taifa hilo la kusini mwa Afrika kama "taifa chafu" na taifa la mabwege.

Botswana imeitaka jumuiya ya kiuchumi ya nchi za kusini mwa Afrika Sadc pamoja na Umoja wa Afrika kushutumu tamko hilo la Trump.

Taarifa ya AU
Umoja wa Afrika, katika taarifa yake Ijumaa ilisema Afrika inasikitishwa na matamshi ya Rais wa Marekani na imemtaka “afute matamshi” hayo na “awaombe radhi Waafrika.”

“Umoja wa Afrika unalaani vikali matamshi yasiyo ya heshima na inamtaka ayafute na pia awaombe radhi siyo tu Waafrika, bali watu wote wenye asili ya Afrika walioko duniani kote,” ilisema taarifa hiyo.

Ebba Kalondo, ambaye ni msemaji wa mwenyekiti wa AU Moussa Faki, mapema aliliambia shirika la AFP kwamba kauli ya Trump “haikubaliki”.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Rupert Colville amesema tamko hilo la Trump ni la kushangaza, la aibu na la ubaguzi wa rangi.

Colville amesema: "Iwapo yatathibitishwa, matamshi haya ni ya kushangaza na ya aibu sana kutoka kwa Rais wa Marekani; nasikitika kwamba hakuna maneno mengine ya kueleza hili ila kusema kwamba ni ubaguzi wa rangi.”

Colville alizungumzia hotuba ya Trump wakati wa kampeni 2016 ambapo alisema wahamiaji kutoka Mexico ni wahalifu na wabakaji. Trump alitoa matamshi hayo alipokutana na wabunge kutoka vyama vyote kujadili pendekezo la mpango wa wahamaiji usiopendelea upande wowote.

Baadaye Trump kupitia Twitter yake alijitetea kwa kusema hakutumia maneno hayo, lakini akasema aliyoyasema alitumia "lugha kali".

Share on Google Plus

About NYEMO FM RADIO

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment