Mamlaka ya mapato (TRA) Dodoma, imesema nyumba zilizokamilika zinatakiwa kulipa kodi ya Majengo kwa mujibu wa sheria.





Mamlaka ya mapato (TRA) mkoa wa Dodoma, imesema Kuwa nyumba ambazo zimekamilika na zinatumika ndizo zinatakiwa kulipa kodi ya Majengo kwa mujibu wa sheria.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mwandamizi wa Huduma na Elimu kwa mlipa kodi mkoa wa Dodoma, Barbanasi John Masika wakati akizungumza na Nyemo Fm, ambapo amesema kuwa nyumba zinatakiwa zifanyiwe uthamini ili kupata viwango maalumu vya ulipaji kodi hiyo.

Masika amesema kuwa uthamini ni hali ya kujua thamani ya jengo au nyumba kwa ajili ya kutoza kodi ya majengo kwani kila nyumba zinatofautiana hivyo, kodi inatozwa kutokana na thamni ya jengo husika, kulingana na mahali lilipo.

Sambamba na hayo ameongeza kuwa, Serikali za mitaa zimepewa jukumu la kuchagua wathamini wa majengo, hivyo mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa kushirikiana nao wanapata wathamini ambao kazi yao kuu ni kujua hali ya jengo na kukadilia tozo yake.

Mamlaka ya Mapato nchini inaelekea katika wiki ya elimu kwa mlipa kodi wiki ambayo itahusisha elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ili kufahamu majukumu ya mamlaka na kutatua changamoto zitakazoibuliwa na wananchi ambapo katika mkoa wa Dodoma wiki hiyo inaanza rasmi tarehe 5 mpaka tarehe 9 mwezi huu katika viwanja vya Nyerere Square vilivyopo katikati ya mji wa Dodoma.

Share on Google Plus

About NYEMO FM RADIO

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment