Mamlaka
ya Mawasiliano (TCRA) imezindua mfumo wa kusajili laini kwa kutumia alama
za vidole.
Mfumo huo ujulikanao kama Baiometria utawezesha
kupata taarifa sahihi za wateja wa kampuni zote za simu nchini, ilielezwa.
Mfumo huo umeanza kwa majaribio katika mikoa sita
ya Dar es Salaam, Tanga, Singida, Pwani, Iringa na Zanzibar, ilielezwa zaidi na
kila mmmoja utakuwa na kituo kimoja cha usajili.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika jana
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba, alisema hatua hiyo
imefikiwa baada ya kuwapo vitendo vya watumiaji wa huduma kugushi vitambulisho
au kutumia vitambulisho vya watu wengine.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, TCRA
kwa kushirikiana na watoa huduma za simu za mkononi na Mamlaka ya Vitambulisho
vya Taifa (Nida) waliazimia kuanzisha mfumo huo.
"Mfumo huu ni wa usajili wa laini za simu kwa
kutumia Baiometria; yaani mfumo wa kuchukua taarifa za wahusika kwa njia ya
alama za vidole. Kama tunavyojua kila mtu ana alama pekee za vidole
zisizofanana na za mtu mwingine yeyote duniani," alisema Kilaba.
Alitaja faida za kutumia mfumo huo kuwa ni kupata
takwimu sahihi za watumiaji wa simu za mkononi na huduma za fedha ambao ni
takribani milioni 22, kwa ajili ya kuweka mipango sawa ya kuendeleza sekta na
uchumi wa nchi kwa ujumla.
Alisema faida nyingine ni kujenga imani kwa
watumiaji wa huduma na kudhibiti matumizi ya laini za simu kufanya uhalifu.
Alisema namba inayosajiliwa kwa majina bandia
inaweza kutumika kutapeli au kutuma ujumbe mfupi wa maneno au simu za matusi na
kuudhi.
"Hii itarahisisha huduma za kuhamia mtandao
mmoja kwenda mtandao mwingine wa simu bila kubadili namba yako, ambayo
ilizinduliwa mapema mwaka jana," alisema Kilaba.
"Kwa upande wa watoa huduma, usajili
utawawezesha kuwajua wateja wao na kuwahudumia kwa ufanisi zaidi."
Vitambulisho vitakavyotumika kusajili alama za
vidole ni cha Taifa, mpiga kura, leseni ya udereva, kitambulisho cha Mzanzibari
Mkazi na hati ya kusafiria.
Chanzo. Mpekuzi
0 comments:
Post a Comment