Ili kukabiliana
na changamoto za kiafya na mazingira Wadau wa Afya mkoani hapa wametengeneza
Mpango wa pamoja wa Afya Kinga ambao utatekelezwa kwenye halmashauri za mkoa ukilenga
kuzihusisha idara mbalimbali za serikali
Hatua hiyo imekuja kutokana uwepo wa changamoto za kiafya,hali
ya mazingira na usafi ikiwemo miundombinu ya vyoo,maji na mabafu kwenye shule
na kaya.
Mshauri Kiongozi wa mradi wa Tuimarishe
Afya (HPSS) ALLY KEBBY akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimishwa
kwa mkutano wa siku mbili wa kimkoa wa uratibu wa shughuli za afya kinga
uliofanyika mjini Dodoma amesema mpango huo umeletwa kutokana na
malengo waliyojiwekea ya kusaidia kuimarisha afya jamii.
Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya, Kitengo cha Elimu ya Afya
shuleni AVIT MARO amesema katika kuboresha afya kinga serikali imeweka miongozo
na sera inayotekelezwa kwenye ngazi mbalimbali..
Nae THERESIA KIWITE kutoka
wizara ya elimu sayansi na teknolojia amesema pamoja na wizara ya Afya
kuandaa miongozo na kuisimamia wamekuwa wakishirikiana katika kuitekeleza.
Mkutano huo umeratibiwa na Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa wa
Dodoma kwa kushirikiana na Mradi wa HPSS-Tuimarishe Afya unaofadhiliwa na
Shirika la Maendeleo la Uswisi(SDC) na kuwakutanisha wawakilishi wa Wizara ya
Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI).
Wengine ni Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Wakuu wa idara za
Elimu, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Idara za Utumishi na Wakuu wa Idara za
Maendeleo ya jamii kutoka Halmashauri za mkoa wa Dodoma.
0 comments:
Post a Comment