Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima ambapo
waumini wanapakwa majivu yanayowakumbusha kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini
watarudi, changamoto kubwa ni kupyaisha maisha ya kiroho kwa njia ya: Sala na
sadaka.
Ni wakati wa kujichimbia katika
tafakari ya Neno la Mungu pamoja na matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii
ni njia muafaka ya kujiandaa kikamilifu ili kukutana na Kristo Mfufuka
aliye hai katika Neno lake, Sakramenti za Kanisa na kwa njia ya huduma makini
kwa jirani sehemu muhimu sana ya mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa
duniani.
Waamini wajitahidi kufunga ili
kuratibu vilema vyao na kwa kuepuka dhambi za mazoea na hatimaye, wamwombe na
kujiaminisha kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwakirimia toba na wongofu wa ndani
unaowaletea upya wa maisha, tayari kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka
baada ya siku 40 za maisha ya kiroho jangwani! Kipindi cha Kwaresima yaani Siku
40 ni safari ya maisha ya kiroho inayojikita katika: imani, matumaini na
mapendo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema,
Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kujiandaa ili kuadhimisha Pasaka ya
Bwana, muda wa neema na kisakramenti cha wongofu wa ndani kinachotangaza na
kutekeleza uwezekano wa kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa moyo na maisha yote! “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo
wa wengi utapoa” (Rej. Mt. 24:12) ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa
Kwaresima kwa mwaka 2018. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu
manabii wa uongo, moyo uliopooza kwa ubaridi; umuhimu wa sala, matendo ya
huruma na kufunga ili kuwasha moto wa Fumbo la Pasaka kwa kuabudu Ekaristi
Takatifu na kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya Sakramenti ya
Upatanisho!
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu
Francisko Siku ya alhamisi, tarehe 15 Februari 2018, kuanzia saa 3:30 majira ya
asubuhi kwa saa za Ulaya atakutana na kuzungumza na Wakleri wa Jimbo kuu la
Roma, kama sehemu ya utekelezaji wa mapokeo ya Jimbo kuu la Roma, ambapo
Wakleri wanakutana na Askofu wao ili kuanza safari katika jangwa la maisha ya
kiroho. Askofu
mkuu Angelo De Donatis, Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Roma anasema, hiki kitakuwa
ni kipindi cha kuadhimisha Liturujia
ya Kitubio cha jumlapamoja na kutoa nafasi kwa wakleri kuweza kujipatanisha na
Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Baadaye, Baba
Mtakatifu atazungumza na Wakleri wenzake kwa faragha, kwenye Kanisa kuu la
Mtakatifu Yohane wa Laterano, mjini Roma.
Askofu mkuu Angelo De Donatis, anawaalika
waamini wa Jimbo kuu la Roma kutafakari kwa kina na mapana kuhusu magonjwa ya
maisha ya kiroho, yaliyopembuliwa wakati wa Kongamano la Kichungaji, Jimbo kuu la Roma, tarehe 18
Septemba 2017 mintarafu: Uchumi unaowatenga watu, saratani ya ubinafsi na
uchoyo; malumbano yasiyokuwa na tija wala mashiko kati ya Wakristo; hali ya
watu kujikatia tamaa ya maisha pamoja na waamini kukengeuka na kumezwa mno na
malimwengu. Kumbe, Kwaresima ni kipindi kilichokubalika kwa waamini kufanya
tathmini ya kina, kushirikishana na kujitakasa, tayari kutoka kifua mbele ili
kutangaza na kushuhudia “Furaha ya Injili”.
Baba Mtakatifu Francisko katika
Waraka wake wa Kitume “Evangelii
gaudium” yaani “Furaha ya Injili” anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi
mema kuondokana kabisa na uchumi unaobagua, uchu wa mali na madaraka na kwamba,
fedha inapaswa kutumika kwa ajili ya huduma na wala si chombo cha kutawala na
kuwanyanyasa watu. Waamini wajitahidi kujenga na kudumisha umoja, usawa, udugu
na mshikamano, sanjari na utamadunisho, ili tunu msingi za maisha ya Kiinjili
ziweze kupenya katika mila, desturi na tamaduni za watu kwa kuondoa yale yote
yanayosigana na Injili ya Kristo ili kupyaisha maisha ya watu!
Baba Mtakatifu
anaikumbusha mihimili ya uinjilishaji juu ya changamoto na matatizo mbali mbali
wanayoweza kukutana nayo katika hija ya maisha na utume wao. Changamoto kubwa
inajikita katika maisha ya kiroho: ubinafsi na utepetevu wa maisha ya kiroho,
hali ya kukata tamaa ya maisha, kwa kuwa na mahusiano tenge na Kristo Yesu,
Bwana na Mwalimu; kwa kumezwa mno na malimwengu, migogoro na kinzani zisizokuwa
na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa. Tafakari hii
iwasaidie waamini kuweza kuwa na sera na mbinu mkakati wa pamoja, utakaoweza
kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Kongamano la Kichungaji,
Jimbo kuu la Roma. Waamini wakumbuke daima kwamba, wagonjwa ndio wanaomhitaji
daktari. Kumbe, wanaweza kutweka hadi kilindini huku wakiwa wamejipyaisha kwa
ari na moyo mkuu, tayari kutangaza Injili ya Fumbo la Pasaka, kwa walimwengu
wote!
Na Padre Richard A.
Mjigwa, C.PP.S.
0 comments:
Post a Comment