Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa
Serikali Dkt. Hassan Abbas akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari
kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Kushoto katika
picha ni Bw. Patric Kipangula Mkurugenzi Msaidizi upande wa usajiri wa
Magazeti.
Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbas akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo wakati alipotoa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Dkt. John Pombe Magufuli na kutolea ufafanuzi wa masuala kadhaa, Kushoto katika picha ni Bw. Patric Kipangula Mkurugenzi Msaidizi upande wa usajiri wa Magazeti na kulia ni Rodney Thadeus Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Maelezo.
&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&&
NIDHAMU mpya katika ukusanyaji na
matumizi ya fedha za umma na dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi kubwa
kwa faida ya wananchi vimesaidia Serikali ya Awamu ya Tano chini ya
Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuendelea kutekeleza kwa mafanikio miradi mbalimbali mikubwa ya kitaifa.
Baadhi ya mambo yaliyotekelezwa na kufafanuliwa leo kwa wanahabari ni
kama ifuatavyo:
Hali ya Uchumi
Kama alivyoeleza Dkt. Philip
Isdor Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango siku chache zilizopita,
tunawahakikishia watanzania kuwa hali ya uchumi wa nchi yetu inaendelea
kuwa imara kwa kiasi cha kuziridhisha taasisi mbalimbali za kimataifa.
Ripoti za Shirika la Fedha
Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya
Marekani zimetabiri kuwa wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa
asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea
kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5
hadi 7.0 katika mwaka 2018.
Ahadi ya Kuhamia Dodoma
Serikali ya Awamu ya Tano
imeendelea kuonesha nidhamu ya kuahidi na kutekeleza ahadi ya kuhamia
makao makuu, Dodoma. Kufikia mwishoni mwa Desemba, 2017, viongozi
waandamizi wa Serikali wameshahamia Dodoma. Rais mwenyewe akitarajiwa
mwaka huu.
Mbali na viongozi, jumla ya
wafanyakazi 3,671 kutoka wizara na taasisi mbalimbali za umma
wameshahamia makao makuu Dodoma. Awamu inayofuata baadaye mwaka huu
itahusisha wafanyakazi wengine 2,460. Sekta binafsi ichangamkie fursa za
Dodoma.
Viwanda Vyashamirisha Uchumi Mpya
Moja ya ajenda kuu za Serikali ya
Awamu ya Tano ni kujenga uchumi mpya wa viwanda. Kufikia mwaka jana
viwanda zaidi ya 3,300 vilisajiliwa kupitia Msajili wa Makampuni (250),
Kituo cha Uwekezaji (361), Mamlaka ya Usimamizi wa Maeneo Maalum ya
Kiuchumi (41) na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO lililosajili
viwanda vidogo vya kati ya mtu mmoja hadi 9 takribani 2,721). Ujenzi na
uzalishaji katika viwanda hivi uko katika hatua mbalimbali.
Kati ya miradi hiyo
iliyosajiliwa, viwanda vikubwa ni 652. Viwanda hivi vina jumla ya mtaji
wa zaidi ya TZS trilioni 5 utakaowekezwa nchini na vitaajiri watu
50,625. Katika taarifa ya mwezi ujao tutaainisha baadhi ya viwanda
vilivyokamilika na uzalishaji unavyoendelea.
Miradi Mikubwa ya Umeme
Katika sekta ya nishati, Serikali
inaendelea kutekeleza miradi zaidi ya 20 ya kuhakikisha nchi ina umeme
wa uhakika. Miongoni mwa miradi ya kimageuzi ni usimikaji wa mitambo ya
umeme wa gesi Kinyerezi I (mtambo wa nyongeza wa megawati 185) na
Kinyerezi II wa megawati 240. Mitambo hii kwa pamoja itaongeza megawati
425.
Mtambo wa Kinyerezi 1-nyongeza
umefikia asilimia 50. Mtambo wa Kinyerezi II umekamilika kwa asilimia 87
ambapo Desemba, 2017, mtambo huo wa kisasa umeingiza megawati 55.94
katika gridi ya Taifa. Kiasi kingine cha megawati 27.94 kinatarajiwa
kuingia kwenye gridi mwezi huu. Mitambo yote miwili itakamilika mwaka
huu.
Ujenzi Reli ya Kisasa “Standard Gauge”
Aidha, Serikali imeendelea
kutekeleza mradi wa kihistoria wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kiwango
cha kimataifa (Standard Gauge) kwa kuanzia na kipande cha kilometa 300
(Dar-Moro) kitakachogharimu TZS trilioni 2.7.
Kazi ya kusanifu njia yote
itakayopita reli imeshakamilika na kwa sasa uandaaji wa tuta, ujenzi wa
madaraja kabla ya kutandika reli yenyewe umeanza kwa kasi. Aidha, ujenzi
wa kipande cha pili cha kilometa 442 (Morogoro-Makutupora, Dodoma)
kitakachogharimu TZS TZS trilioni 4.3, mkandarasi ameshaanza maandalizi.
Ununuzi Mabehewa, Vichwa Waanza
Wakati ujenzi wa reli ukiendelea,
Serikali kupitia Kampuni Hodhi ya Raslimali za Reli (RAHCO)
imeshatangaza zabuni kwa ajili ya kupata makampuni yatakayotengeneza
vichwa na mabehewa ya kisasa ya treni ya umeme na mafuta. Zabuni
zitafunguliwa mwezi huu.
Katika zabuni hiyo Serikali
inatarajia kununua vichwa 25 (23 vya umeme na 2 vya dizeli), mitambo 25
ya ukarabati wa reli na mabehewa 1,590 (kati ya hayo 1,530 yakiwa ni ya
aina mbalimbali za mizigo kama vile kubeba makontena, nafaka, mafuta
n.k), mabehewa 60 ni ya abiria (15 yakiwa ni daraja la kwanza na 45
daraja la kawaida).
Meli Mpya Zaleta Matumaini Maziwa Makuu
Serikali iliahidi na sasa
inatekeleza. Katika Ziwa Nyasa mwishoni mwa wiki iliyopita meli mbili
mpya za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma zinazobeba mizigo tani 1,000
kila moja zimeanza safari kwenda bandari mbalimbali zikiwemo za nchi
jirani. Serikali imetumia TZS Bilioni 11.252 na meli nyingine mpya ya
abiria itakamilika Juni mwaka huu.
Katika Ziwa Victoria, kupitia kampuni ya Serikali ya Huduma za Usafiri Katika Maziwa, Marine Services Company LTD, mkandarasi wa kutengeneza meli mbili kubwa, mpya na za kisasa ameshapatikana. Aidha, tayari meli ya abiria ya MV Clarios na ya mizigo MV Umoja zilizofanyiwa ukarabati na kuwa za kisasa zimeshaanza kazi.
Katika taarifa zijazo tutaendelea
kutoa maendeleo ya miradi hii mikubwa na kuainisha utekelezaji katika
sekta na miradi mingine kwa wananchi. Kwa maelezo zaidi kuhusu taarifa
ya leo ikiwemo picha za miradi zinazoambatana na taarifa hii tafadhali
tembelea:
Tovuti: www.maelezo.go.tz
Blogu: www.blog.maelezo.go.tz
Twitter: TZ_Msemaji Mkuu
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi, Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
0 comments:
Post a Comment