Msanii Suzan Michael maarufu kama Pretty Kind afungiwa kujihusisha na sanaa kwa muda wa miezi sita.




Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza amemfungia msanii Suzan Michael maarufu kama Pretty Kind kujihusisha na sanaa kwa muda wa miezi sita.

Akizungumza leo Jumapili Januari 7 jijini Dar es Salaam, Shonza amesema amechukua hatua hiyo kutokana na msanii huyo kutoa wimbo uitwao ‘viduduwasha’ usio na maadili.

Msanii huyo pia amekutwa na kosa la kufanya kazi ya sanaa bila kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), kuweka mtandaoni picha ya nusu utupu kinyume na maadili.

‘’Kumekuwa na wimbi kubwa la wasanii kutoa nyimbo zenye maneno ya matusi na zisizo na maadili, pamoja wanawake kupiga picha wakiwa wamevaa nusu utupu na kuweka picha hizo katika mitandao,” amesema Shonza na kuongeza,

“Nataka kuwapa angalizo wasanii wenye tabia hizi kuwa Serikali inawafuatilia kwa karibu na mwaka huu tumeanza na huyu na wengine wanafuata kama msanii Gift Stanford maarufu kama Gigy Money na Jane Rimoy maarufu kama Sanchi.”

Shonza amemtaka msanii Gigy Money kufika ofisini kwake haraka, kwa maelezo kuwa alimtaka afanye hivyo siku za hivi karibuni lakini ameshindwa kuitikia wito wake.

Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza amesema kwa mujibu wa kanuni 31 (1) ya baraza ya mwaka 2005, inaeleza msanii kufanya kazi bila kusajiliwa ni kosa na anaweza kufungiwa, pia kwa upande wa mavazi zinasema msanii anatakiwa kuvaa mavazi yenye staha yasiyomdhalilisha wala kudhalilisha watazamaji wake.

“Napenda kuwasisitiza wasanii wote ambao wanajijua kuwa hawajasajiliwa Basata kuja kujisajili haraka na kwa wale waandaji wa kazi za sanaa kama waongozaji, waandaaji na wamiliki wa studio za kurekodi kazi za sanaa ambao hawajasajiliwa nao waje kujisajili haraka,” amesema.
Chanzo-Mwananchi

Share on Google Plus

About NYEMO FM RADIO

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment